LUGHA YA KISWAHILI


 Huu ni ukurasa maalum unaokuletea habari na taaluma ya kutosha juu ya lugha ya kiswahili ,kabila la waswahili na tamaduni zao.

WASWAHILI KABILA LILILOZIKWA.

KISWAHILI, neno kiswahili linaposikika kwenye sikio la msikilizaji huamsha ari nyingi na hamasa kubwa ya kutaka kujua hasa ni nini kinazungumzwa kuhusiana na lugha hii.

Mengi yameelezwa na kufafanuliwa kuhusu lugha ya kiswahili kwa mapana na marefu.Vitabu chungu tele vimeandikwa katika lugha hii ya kiswahili vikielezea historia fasihi pamoja na sarufi ya lugha hii.

Ama kwa hakika jambo moja kubwa na la kushangaza ni kana kwamba lugha hii imetokea bahati mbaya au ni lugha iliyojikusanya na kujiungaunga mpaka ikawa hivi ilivyo yenyewe pasi na kuoneshwa kuwa kuna wenyewe wenye lugha yao.

Katika tafiti mbalimbali za elimu ya mambo ya kijamii zinapozungumzia juu ya suala la lugha basi lazima kuwe na sehemu ambayo ndio asili ya kabila hilo na lugha husika.Hakuna lugha inayochipua bahati mbaya,kila lugha ina asili na mahali pake.Jambo hili ndilo linalonishangaza sana kuona kikijadiliwa sana kiswahili na tafiti chungu tele zikiandikwa huku watafiti hao wakisahau kunena ukweli kuwa lugha hii asiliye ni kabila la waswahili.

Hapa ndipo ninapoanzia kudadavua kuhusu hili ambalo halitaki kuelezwa wala kusemwa na limekaliwa kimya muda mrefu.Wapo wanaodai kuwa waswahili si kabila alaa! kama kitu hukijui sema sikijui usiseme hakipo ili utakaposema hukijui tutakufahamisha na hatimaye utakijua.

Ama kwa hakika WASWAHILI tupo na hili ni kabila lenye miaka mingi asili na azali kabila kongwe lilitamalaki katika upwa wa mwambao wa bahari ya hindi mwa Afrika mashariki.

Haiyumkiniki kuwepo na lugha kusiwe na kabila wanayoisema lugha hiyo lahasha ninakataa ni jambo lisilowezekana.

Zipo hoja nyingi tu anuai zinazooenesha kuwa kabila la WASWAHILI lipo nalo ni lile linaloishi katika upwa wa mwambao mwa bahari ya hindi Afrika mashariki.Kabila hili limeanzia mbali sana kuambaa na mwambao wa bahari ya hindi.Katika nchi ya Tanzania na Kenya kabila hili hupatikana ukanda wa:-

Kilwa,Somanga,Lindi,Mtwara,Bagamoyo,Saadani,Mkwaja, Mwera,Sakura,Kipumbwi,Pangani,Kigombe,Mwarongo,Tongoni,Machui,Kiwavu,Kivindani,Chongoleani,Mnyanjani,Ndumi,Kwale,Monga,Vyeru,Manza,Moa,Kijiru,Vanga,Jasini,Ramisi,Mijikenda,Pate,Lamu,Shungwaya na sehemu kubwa ya mwambao huu vikiwemo visiwa vya Tumbatu,Pemba na Unguja humu mote ndimo waiishimo WASWAHILI.

Ukifanya utafiti mdogo wa kubaini matamshi ya asili ya lugha ya kiswahili mengi yamo katika lahaja zinazopatikana katika lahaja za ukanda huu nilioutaja.


Ujio wa wageni Waarabu,Wareno,Wajerumani na Waingereza unathibitisha wazi kabisa kuwa watu wa mwambao huu wa Pwani ya Afrika mashariki walikuwa na lugha yao ambayo ilikuwa ikiingiliana kwa kiasi kikubwa sana na walikuwa wakiitumia katika shughuli zao za kila siku na tamaduni zao pamoja na mawasiliano yao.

Hata maandishi ya awali mfano kitabu cha tenzi tatu za kale kiliandikwa kwa lugha ya kiswahili ambayo ndiyo ilikuwa lugha ya WASWAHILI.

WASWAHILI ni kabila lina utamaduni wake mwingi sana.Kabila la waswahili limejishughulisha sana na shughuli za ukulima uvuvi na ufugaji na pia hujulikana kuwa ni watu mashujaa na shupavu katika vita.

WASWAHILI ni kabila linalopenda sana kufanya biashara hasa kusafiri, kabla ya ujio wa wageni walikuwa wakisafiri kutoka pwani hadi bara kwa shughuli zao mbalimbali pia walikuwa wakitumia zaidi ngalawa na mashua  kufika sehemu mbalimbali katika bahari ya hindi na hata kusini mwa Afrika kwa shughuli zao za uvuvi.

WASWAHILI walikuwa na mfumo wao wa uongozi au utawala uliokuwa ukijulikana kwa jina la UMWINYI.Jamii imelielewa vibaya sana neno hili.Kiongozi katika kabila la waswahili huitwa MWINYI na utaratibu mzima wa uongozi huitwa UMWINYI umwinyi sio uvivu.

WASWAHILI ndio wenye lugha ya kiswahili.Hata ilipotaka kusanifiwa lugha hii ili iweze kutumika kwa mawanda wakati wa utawala wa muingereza lahaja ya kiunguja ndio iliyochaguliwa.

Wasanifishaji waliitafuta moja miongoni mwa lahaja ya WASWAHILI iliyoingiliana na lahaja  nyingi ndipo ikateuliwa ambayo nayo ni LAHAJA YA KIUNGUJA. Lahaja hii ukiambiwa kuwa ilikuwa ikiingiliana sana maneno yake na lahaja nyingine ni kuwa hizo lahaja nyingine ndio hizo zinazopatikana katika upwa wa Afrika ya mashariki.

Kitu kilichowashinda ni kukiri na kukubali ukweli kuwa wakazi wa upwa wa Afrika mashariki ambao ni kabila la WASWAHILI walikuwa na lugha yao toka azali kama makabila mengine.Watafiti wengi wanapindisha ukweli huu na kutaka kuonesha kuwa kiswahili ni lugha iliyozuka kwa kuungaunga maneno.

Ukweli utabaki kuwa ukweli hata siku moja ukweli hauzami.Jamii ya watu wa mwambao wa Pwani ya Afrika mashariki toka mtu amezaliwa mpaka anakuwa hana lugha anayoijua wala kabila analolijua isipokuwa kiswahili na uswahili.

Sawa tuseme watu wa ukanda wa Tanga wanaongea kimtang'ata hebu kisikilize halafu kiweke na kiswahili ukipime je kinaachana, katu hata siku moja tofauti ni ndogo tu ya mpishano wa msamiati na matamshi.

Wasomi wengi sana wamejaribu kuchambua kitabu cha TENZI TATU ZA KALE na kilichowastaajabisha wakikisoma kiswahili kilichoandikwa humo hawayaelewi wala hawayapatia maana ya maneno yaliyomo, waseme ukweli waliwezaje kung'amua maneno yaliyomo katika kitabu hicho ni kuwa waliamua kutembelea jamii ya WASWAHILI wenye lugha yao na ikawa inawafahamisha maana ya neno moja baada ya jingine.

Vijana wengi ambao ni wazaliwa wa ukanda wa pwani kama nilivyo mimi ukiniuliza kabila langu napata tabu sana kujua mara nasema mdigo mara msegeju nilipoamua kupita na kufanya utafiti binafsi kubaini mimi ni kabila gani ndipo nilipojuwa kuwa mimi ni MSWAHILI wa MOA TANGA wala si mdigo na wala si msegeju. Hili ndilo lililonifanya kuibua hii hoja ya kabila la WASWAHILI .

Na ninaposema watu wanaoishi katika mwambao wa bahari ya hindi mwa pwani ya Afrika mashariki naomba nieleweke kuwa hawa ni wale wote tu wakiamka asubuhi basi wao macho yao yanaona bahari na kusikia vumo la pepo za bahari na mawimbi yake.Hawa ndio niwasemao kuwa hawa ni WASWAHILI.

Hoja yangu nahitimisha na kusema 

HAKUNA LUGHA INAYOKUWEPO NA IKATUMIKA PASI NA KUWEPO KABILA LAKE.

WASWAHILI LUGHA YAO NI KISWAHILI.

Nitaendelea...........fuatilia na tembelea ukurasa huu kwa  ajili ya kupata mengi juu ya MSWAHILI na UTAMADUNI wake.

No comments:

Post a Comment