Wednesday 28 September 2016

TANGA NA UTALII

TANGA NA FURSA YA UTALII

Katika sekta ya utalii ni kama vile mji wa Tanga umesahaulika katika nchi ya Tanzania.Wengi wakielezea hutalii huelezea zaidi juu ya mbuga za wanyama na haswa hicho ndio kimefanywa kuwa ndio kivutio kikubwa cha utalii au uwepo wa mambo ya kale.Jambo hili ni upotofu wa hali ya juu.

Suala la utalii ni pana mno na utalii umegawika katika makundi anuai :

Utalii wa uwanda wa ardhi:Hii ni aina ya utalii ambapo watalii huajabia namna umbile la ardhi la sehemu fulani lilivyo mfano uwepo wa ardhi tambarare yenye nyasi ndogondogo au uwepo wa ardhi tambarare yenye changarawe ambayo imeenea eneo kubwa au uwepo wa milima mambonde makubwa yenye kustaajabisha ni vivutio vya utalii.

Tanga kwa hili tuna milima ya usambara ambayo INA jiografia kubwa na ya kuvutia Juhudi za kuitangaza LUSHOTO na AMANI katika kivutio hiki bado iko chini sana kiasi cha kuifanya TANGA kuonekana kama vile suala la utalii halina nafasi.

Utalii wa mito: Maporomoko ya maji kutoka katika maeneo ya juu ya mito ni kivutio kikubwa sana katika sekta ya utalii.Hili huonekana kama vile halina nafasi Tanga na kuonekana kama vile hakuna mito mikubwa na yenye maporomoko ya kustaajabisha kumbe Tanga tuna mto zigi ambao ndio tegemeo la maji ya kutumia katika jiji la Tanga mto huu hutokea juu kabisa kwenye milima ya usambara ambapo chemchem yake ndipo ilipoanzia.

Tuna mto Pangani ambao huu nao una mchango mkubwa katika kuzalisha umeme wa Taifa hili MTO huu mlango wake wa kuingilia bahari ya hindi hukutana na bahari na hakika maji ya mto huu hayachanganyiki na maji ya bahari.

Wangapi washalitangaza hili wangapi washalifanyia utafiti hili na kutangaza kivutio hiki cha utalii?

Maporomoko ya maji yaliyopo milima ya usambara nani ameyatangaza? Kituo cha kuzalisha umeme wa maji cha Pangani kilichopo Hale je ni nani amekitangaza? Kwa kawaida sekta ya utalii hukua katika eneo husika kulingana na namna wana jamii wanaoishi katika eneo husika wanavyoutangaza utalii wa kwao.Tusione maeneo yenye mbuga za wanyama kuwa ni kivutio kikubwa cha utalii ni kwasababu wenyeji wa maeneo hayo waliamua kuutangaza utalii huo na kuufanya kuwa ni sehemu ya ajira na kuwaingizia kipato.

Utalii wa bahari : Mungu katujaalia kuwa na fukwe kubwa sana lakini mpaka sasa utalii wa bahari bado haujajulikana na kutangazwa .Utalii wa bahari kuna visiwa vingi ndani ya bahari ya Hindi ukanda wa Tanga Tanga ambavyo vina historia kubwa na maajabu mengi sana mfano KISIWA MWEWE pwani ya MOA, KISIWA CHA MTANG'ATA PWANI YA TANGA,KISIWA CHA FUNGUNI PWANI YA TANGA  kama hatutaamua kuitangaza Tanga yetu na utalii hakuna atakayekuja kututangazia.

Utamaduni wa uvuvi na namna ya kuvua ni sehemu mojawapo ya utalii wa bahari ukanda wa Tanga una utamaduni wa asili katika kuvua ambapo ukiwaona wavuvi wakiitekeleza shughuli hii kwa tamaduni zao huwa ni yenye kuvutia .Nani atautangaza utalii wa Tanga kama sio mimi na wewe.? Migodi ya utengenezaji chumvi kilimo cha mwani hivi vyote ni vivutio vya utalii wa bahari.Fukwe ambazo tunazo ndani ya Mkoa huu wa Tanga zenye mandhar nzuri na za kuvutia lakini je zimetangazwaje? Tunashuhudia watu husafiri kuajabia ziwa Victoria lakini huwaoni kusafiri kuajabia maajabu ya bahari ya hindi katika upwa huu wa Tanga.Hii ni kwasababu hatujaamua kuifanya Tanga kuwa ni sehemu ya utalii.

Utalii ni tasnia inayotengenezwa,haitoshi tu kuwa na mazingira asilia bali ni kwa kiwango gani mazingira hayo yametengenezwa kuwa kivutio cha utalii?

Angalia utalii wa bahari unavyotengenezwa

Moja ,uwepo wa fukwe , ni lazima pia kuwepo na vifaa vya michezo na michezo inayoambatana na utalii wa fukwe kama viwanja vya michezo kandokando ya fukwe.Viwanja hivi huwa na mazingira yaleyale ya asili na hufuata kanuni zote za uhifadhi wa mazingira ya fukwe.

Pili, vifaa vya kuchezea majini kama ngalawa boya hizi ni ngalawa maalum ambazo hutumiwa kuchezea michezo ya ndani ya maji kwa kuyakata mawimbi.

Tatu, uwepo wa hotel nzuri za kisasa na zenye mandhari ya pwani zinazozingatia gharama kwa mtuvwa ndani na mgeni kutoka nchi nyingine.MFANO tunaona TICC MCHUKUUNI wamejaribu kufanya kitu cha namna hii na wageni huja wengi tu kuajabia mazingira ya bahari.

Bwawa la viumbe vya baharini, ni lazima kuwe na bwawa kubwa sana lililojengwa katika mandharu ya kuvutia ambapo linaweza kumsaidia mtu kuona kila aina ya samaki waliomo baharini na maisha yao kwa ujumla.Katika kulindeleza hili baadhi ya nchi wamejenga hotel ambazo ukiingia unaiona sehemu ya maji ya bahari na viumbe mbalimbali hili nalo ni sehemu mojawapo kubwa ya utalii wa bahari.Dubai katika utalii wa bahari wamefanikiwa mno.

Utalii wa mambo ya kale na utamaduni wa eneo husika.Tanga INA historia kubwa sana ndani ya nchi hii ya Tanzania lakini kwa kutoelezwa historian hiyo katika muktadha wa utalii ni kama vile imevizwa.Tuna makaburi ya wajerumani,Waingereza nakadhalika haya yakuelezwa katika muktadha wa utalii tayari tosha huwa ni kivutio cha utalii sisi ni matajiri w mambo ya kale lakini tumejidharau kwenye hili hakuna atakayetujua.Angalia mathalani Shule ya kwanza ya msingi Tanzania wakati huo Tanganyika ni Magila Shule ya kwanza ya sekondari ni Old Tanga nani kaziwekea sura ya utalii vitu hivi? Manispaa ya kwanza Tanganyika au Deutch Osta Afrika ilikuwa ni Tanga Nani kaiwekea sura ya utalii ?

Tuna kuta kubwa sana maeneo ya vijiji vingi vya pwani mathalani moa lakini je ni Nani kazielezea kuta au ngome hizi zilikuwa ni za nini?

Je waijua mashine ya kusaga unayotumia nguvu ya maji ambayo ilijengwa wakati wa mjerumani na mpaka leo hutumika kusaga nafaka eneo la mto zigi Amani? Je wajua kuwa kuna maua na miti pamoja na ndege ambao duniani kote hakuna wanapatikana Amani tu katika Mkoa wa Tanga?

Mwisho kabisa niseme kuwa hakuna mji unaokuwa kiutalii kama haujatangazwa na wenye mji husika na pia kama mazingira asilia yaliyopo hayajaekewa miundombinu ya kuufanya utalii ufanyike kwa kiwango cha hali ya juu.

Amarison Consultancy imedhamiria kuandaa vipindi vya TV kwa jili ya kuutangaza utalii wa Tanga na kila wilaya itatangazwa na kufamika vivutio vyake vya utalii tunaendelea kutengeneza vipindi vyetu wakati ukifika tutahitaji udhamini wa kuvirusha hewani kwenye TV  yoyote ile baada ya kutimiza vigezo na masharti.


              




Friday 23 September 2016

TANZANIA YASHINDA KESI DHIDI YA IPTL

Uamuzi wa ICSID kuhusu IPTL mshindi Ni Tanzania

Septemba 12, 2016 Mahakama ya Usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji iliwasilisha rasmi maamuzi yake Kwa pande zilizokuwa kwenye mgogoro kuhusu mradi wa kufua umeme Nchini, IPTL. Mahakama hiyo iliamuru kwamba Benki ya Standard Chartered ya Hongo Kong ( SCB-HK ) ilipwe dola za Kimarekani 148 milioni sawa na Fedha za Kitanzania shilingi 320 bilioni. Mahakama hiyo Pia imeamuru kuwa kuchotwa Kwa Fedha kutoka akaunti maalumu ya TEGETA Escrow hakukuondoa Haki ya ya Benki ya SCB-HK kwenye kampuni ya IPTL na hivyo kisheria kwamba Benki hiyo Kwa sasa ndio mwenye uhalali wa shughuli zote za IPTL.

Ilinichukua Siku takribani 2 kusoma na kusoma tena tuzo hii (Award ) ili kuweza kuielewa haswa maana yake Kwa Nchi yetu. Ikumbukwe kwamba niliongoza Kamati ya Bunge iliyoagiza uchunguzi wa sakata la TEGETA Escrow Account na kuandaa Taarifa Maalumu ya Kamati ya PAC iliyosomwa na kukubaliwa rasmi na Bunge na kupitisha maazimio 8 yaliyopaswa kutekelezwa na Serikali. Baada ya kuisoma Kwa kina Tuzo hiyo ya ICSID nilichoona Ni kwamba masuala Yale Yale ambayo PAC iliyafafanua Bungeni Mwezi Novemba mwaka 2014 ndio hayo hayo yaliyopelekea tuzo hiyo. Kwa maana hiyo Ni kwamba iwapo Serikali ingetekeleza Maazimio ya Bunge yote Leo hii tungekuwa kwenye nafasi nzuri sana ya kulimaliza suala Hilo kabisa na kuachana kabisa na mgogoro huu ambao unanyonya Fedha za Watanzania.

Kuna masuala makuu 2 ambayo yakieleweka suala la kashfa ya IPTL litakuwa limeeleweka na maamuzi yanaweza kufanyika kumalizana nalo.

1. baada ya mbia ya kampuni ya Mechmar kufilisika nchini Malaysia, Ni Nani mwenye Haki na Mali za IPTL?
2. Tozo ya malipo ya umeme uliozalishwa na IPTL ilizidishwa?
Kwenye Taarifa ya Kamati ya PAC tulionyesha Kwa vielelezo na ushahidi kwamba kampuni ya PAP haikuwa ina umiliki wa kihalali wa asilimia 70 ya Hisa za IPTL. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alionyesha dhahiri kuwa vyeti vya Hisa ( shares certificates ) za kampuni ya Mechmar kwenye IPTL walikuwa nazo Benki ya SCB-HK Kama dhamana ya mkopo waliowapa IPTL. CAG aliziona hati hizo Kwa macho yake kwenye uchunguzi wake ambao ndio uliotumika na PAC kufikia maazimio 8 ya Bunge.

Vile vile Kamati ya PAC ilionyesha Kwa ushahidi kuwa PAP hawakufuata sheria za Tanzania katika kumiliki IPTL ikiwemo kwamba walikwepa kodi kupitia kampuni iliyoitwa PiperLink ya British Virgin Island. TRA walikiri mbele ya Kamati kuwa wakati Mahakama Kuu inatamka kuwa PAP wapewe ' masuala ( affairs ) ya IPTL ) hawakuwa na uhalali wa kufanya Biashara Tanzania kwani hawakuwa wamepewa kibali na Kamishna Mkuu wa Kodi cha kuthibitisha utwaaji wao wa kampuni ya IPTL. Hivyo Kamati ililiambia Bunge kuwa PAP ni matapeli wa Kimataifa waliopiga ganzi Mfumo wa Serikali ya Tanzania Kwa kutumia rushwa na hivyo kuhalalishiwa umiliki wa IPTL ili kuchota Fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya TEGETA Escrow Benki Kuu ya Tanzania.

Hata Gavana wa Benki Kuu alipowaomba PAP uhalali wa wao kumiliki IPTL walichotoa ni kitu kinachoitwa Deed of Assignment badala ya shares certificates. Watanzania watakumbuka kuwa Deed of Assignments ndizo zilizotumika kuiba Benki Kuu kwenye wizi wa EPA mwaka 2004-2005. Jambo la kushangaza Ni kwamba karatasi hiyo ya kugushi ilikubaliwa na hivyo Bwana Harbinder Singh Seth wa PAP akaruhusiwa kuchota mabilioni ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Kwa mujibu wa Mwanasheria wa TANESCO Bwana Richard Rweyongeza TANESCO waliilipa PAP $245m Sawa na shilingi 530 bilioni. Itakumbukwa kuwa wakati PAC inasoma Taarifa yake Fedha hizo zilikuwa tshs 306 bilioni tu.

Katika tuzo yake ICSID imethibitisha kuwa PAP hakuwa mmiliki wa IPTL na hivyo alilipwa Fedha za TEGETA Escrow kimakosa. Hoja hii imethibitisha Hoja ya PAC na Bunge la Tanzania ambayo ilipingwa vikali na Serikali ya wakati huo ambayo iligeuka mtetezi wa PAP. Uamuzi wa ICSID kwamba TANESCO wailipe SCB-HK unathibitisha kuwa PAP alipewa Fedha za TEGETA escrow kitapeli.

Baada ya kumaliza hoja hiyo twende Hoja ya pili; je Hata Kama PAP wangekuwa Ni Wamiliki halali wa IPTL walilipwa ziada?

Itakumbukwa kwamba PAC ililiambia Bunge kuwa mgawo wa Fedha ulipaswa kusubiri kukokotoa kanuni za mgawo ambazo ziliamriwa na Mahakama hiyo ya ICSID. Hoja kubwa ya PAC ilikuwa ' Ni Kwanini tulifanya haraka kutoa Fedha kabla ya Uamuzi wa kiwango gani kilipwe? '. Hoja hii ndio iliyochagiza kuwa mule ndani ya TEGETA escrow kulikuwa na Fedha za umma. Uamuzi wa kukokotoa ukatolewa Mwezi Februari mwaka 2014 lakini katika mjadala mzima wa sakata la TEGETA escrow Serikali ilikataa kata kata kutekeleza Uamuzi huu. Hata kwenye Hoja za TANESCO mahakamani huko hawakuwa kabisa na Hoja kulinda Uamuzi ule. Hata hivyo ICSID imeamua kuwa tulikuwa tunaliwa Kwa kulipa tozo kubwa zaidi ya kiwango tulichopaswa kulipwa. Hii maana yake Ni kwamba Hata kwenye hizo za wizi tuliilipa PAP zaidi ya tulichopaswa kuwalipa.
Katika magazeti ya Leo wakili aliyeiwakilisha TANESCO anasema " tulibishania Hoja ya kulipa Kwa viwango vya zamani ikaamuriwa hesabu zifanyike upya Mahakama iliamuru hesabu zifanyike upya Kwa kutumia mkopo wa wana Hisa ". Hii ndio Hoja ambayo PAC iliijenga Kwa muda mrefu na kubezwa na Serikali ndani ya Bunge Kwa mbwembwe zote. Wakili wa TANESCO anaendelea " kutokana na hesabu hizo gharama ilikuwa chini. IPTL ililipwa zaidi hivyo inatakiwa kurejesha Dola za Marekani zaidi ya milioni 100 Kwa TANESCO ".

Hii ndio ilikuwa Hoja ya PAC ambayo ilitokana na maagizo ya CAG kwamba TANESCO wakae chini na SCB-HK kupiga hesabu upya. Hoja hii ilikataliwa na Serikali na TANESCO wenyewe ilipotolewa na PAC lakini Leo mwanasheria wa TANESCO aliyeiwakilisha TANESCO katika Mahakama ya Usuluhishi ya ICSID anakiri tuliwalipa zaidi IPTL.

Jambo la kushangaza Ni kwamba, licha ya ushindi huu mkubwa Kwa Tanzania na TANESCO wanasheria wanataka tukate rufaa. Magazeti ya Serikali ya Dailynews na habari leo ndio yameongoza na habari hiyo. Ikumbukwe kuwa magazeti hayo ndio Siku zote yamekuwa yakiitetea pap na Bwana Seth. Ni dhahiri kuwa ama wanasheria wanataka waendelee kulipwa Fedha kwenye kesi au kuna shinikizo kubwa kutoka Kwa wanaofadika na mchezo huu wa kutapeli ili waendelee kufisadi Nchi. Uamuzi huu wa ICSID unatuweka kwenye nafasi nzuri sana ya kulimaliza kabisa suala la IPTL kwani umetuonyesha kuwa;
1)Kwa miaka yote ya uwepo wa IPTL tumekuwa tunapigwa Kwa kulipa capacity charges Mara mbili ya kiwango tulichopaswa kulipa
2)Tulitapeliwa na Bwana Seth kupitia kampuni ya PAP ambayo Wamiliki wake wengine 50% mpaka sasa hawajulikani Ni kina Nani licha ya kuwajua Kwa jina la Simba Trusts ya Australia.  

Wakati wanasheria na baadhi ya maofisa wa Serikali waliofadika na mgawo wa TEGETA escrow wanataka kukata rufaa wanajua kuwa maamuzi ya ICSID hayana rufaa Kwa mujibu wa Ibara ya 53 ya mkataba wa ICSID ( no appeal except those provided for in the ICSID Convention ). Hadhi  yake Ni Sawa na maamuzi ya Mahakama ya juu kabisa ya Tanzania Kwa mujibu wa Ibara ya 54 ya mkataba wa ICSID ( convention ). Hata hivyo maamuzi hayo yanaweza kuombewa kufutwa Kwa kutumia Ibara ya 52(2) Kwa sababu maalumu ambazo Ni

a). Baraza la Usuluhishi halikuundwa kisheria ( properly constituted ). Ijulikane kuwa Baraza hili huteuliwa na washiriki wa kesi. SCB-HK waliteua msuluhishi wao, TANESCO waliteua wao na Kwa pamoja wakateua Rais wa Baraza. Hivyo TANESCO hawana Hoja maana Hata msuluhishi waliteua wao kakubaliana na maamuzi haya ya tuzo hii.
b). Kwamba Baraza lilienda nje ya mamlaka yake. TANESCO walishiriki mwanzo mwisho na hawakuwa na malalamiko kuhusu Hilo wanawezaje kuwa na malalamiko sasa. Hata msuluhishi wao kakubali maamuzi haya.
c). Kwamba kulikuwa na rushwa kwenye kufikia maamuzi haya. TANESCO wanaweza kutoa ushahidi Kama Hata msuluhishi waliyemteua wao alihongwa!
d) kwamba tuzo haina sababu za kufikia maamuzi haya. Kwa walioisoma tuzo hii wanajua kuwa sababu zipo kinagaubaga kabisa.

Kwa maoni yangu kutaka kesi iendelee Ni kutaka kulinda maslahi ya wanaofadika na suala zima la IPTL. Suala hili sasa liishe. Nchi imeshaliwa sana. Itoshe.

Ushauri wangu Kwa Serikali Ni Kama ifuatavyo

1. Kutekeleza tuzo hii ya ICSID bila kusita
2. Kuiamrisha kampuni ya PAP kurejesha Fedha zote za ziada ilizolipwa kutoka akaunti ya TEGETA escrow. Kwa mujibu wa tuzo hii Ni jumla ya tshs 202 bilioni
3. Kuitaka kampuni ya PAP kuilipa Benki ya SCB-HK kutokana na hati iliyowasilisha Benki Kuu kwamba madai yeyote yakitokea katika IPTL PAP ndio watalipa ( indemnity ).
4. Kuchunguza na kuishtaki PAP na Bwana Harbinder Singh Seth Kwa utapeli na utakatishaji wa Fedha Kwa mujibu wa sheria za Tanzania
5. Kuchunguza na kuwashitaki maofisa wote wa Serikali walioshirikiana na Seth kuchota Fedha Benki Kuu
6. Kuilipisha faini Benki ya StanBic Tanzania Kwa kushiriki kwenye vitendo vya kutakatisha Fedha kufuatia miamala ya TEGETA escrow
7. Kufunga kabisa suala la IPTL Kwa kuvunja mkataba na kuitwaa mitambo Kwa mujibu wa sheria za Tanzania

Natumai kuwa watu wenye nafasi za Uongozi wa umma ambao maamuzi Yao yamefikisha Nchi hapa watachutama na kuondoka katika Uongozi wa umma. Tumefikishwa hapa na wizi na tamaa za watu madalali wa matapeli. Ninaamini kuwa Rais John Pombe Magufuli hatakubali Nchi hii kuendelea kupigwa na matapeli.

Zitto Kabwe, Mb
Kigoma Mjini

JK APEWA TUZO

HONGERA MH JAKAYA KIKWETE


Rais mstaafu Dk JM Kikwete ametunukiwa Tuzo  Maarufu ijulikanayo kama SPEAKUP AFRICA. Tuzo hii hutolewa kwa watu maarufu na mashuhuri ambao wamethibitika kutoa mchango katika bara la Afrika.

Miongoni mwa viongozi wa Afrika waliotunukiwa Tuzo hiyo ni pamoja na Waziri wa afya na masuala ya kijamii wa Senegal,  Prof Awa Mariel Coll-seck.

Hafla hii ya kuwatunuku Tuzo hiyo imefanyika 22 Sep  2016, katika ukumbi wa American Museum of Natural History, New York, nchini Marekani.

Hongera JK,  Hongera CCM,  Hongera Tanzania kwa kuendelea Kutambuliwa na Ulimwengu kwa Mchango wenu katika Jamii

Kidumu Chama Cha Mapinduzi

Magoiga SN-Mwanza
Mwenyekiti wa Muda-CCM Tawi la Mitandaoni

Thursday 22 September 2016

USIONE UKADHANI ATCL IMETOKA MBALI

KAMA HUJUI SEMA SIJUI UFAHAMISHWE SIO KUPINGA KILA JAMBO

NAIPONGEZA SERIKALI KWA KULIFUFUA SHIRIKA LA NDEGE LA ATCL NA HUU NI MWANZO MZURI.

Kundi kubwa sana la vijana waliopo vyuoni wengi wamezaliwa miaka ya 1990 na kuendelea ,  yaani wakati wanazaliwa ni miaka miwili ndio nchi ya Tanzania inakubali kuwa na siasa za upinzani hivyo hawakuona utawala wa Mwl Nyerere Mzee Mwinyi wengi wamebaleghe utawala ukiwa ni wa mzee Mkapa kwa hiyo wanamengi ambayo hawayajui kuhusu Tanzania.

Kuna haja kubwa sana ya vijana kujengewa uwezo wa kuifahamu historia ya uchumi ya mashirika mbalimbali ndani ya Tanzania maana wanapoona shirika likifufuliwa au kama lilipoteza muelekeo basi huanza kupinga na kudharau jitihada za serikali.

Wamelishwa propaganda za kudharau kila jambo jema la serikali katika jitihada na harakati za kufufua sekta mbalimbali za uchumi wa Taifa hili.

Hapo awali tulikuwa na shirika la ndege tangu wakati wa Mwl Nyerere MZEE mwinyi na lilikuwa likifanya kazi vizuri uwezo wa shirika uliingia kipindi kigumu baada ya kufa JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI.

Ufuatao ni muhtasari wa kuyumba na kulifufua au kulipa uhai shirika hili ili liweze kuwa sehemu mojawapo ya chanzo cha mapato ya Taifa letu.

Kwa kifupi nchi yetu ilianza kusimama pekee kwenye shughuli za anga baada ya kuvunjika iliyokuwa jumuiya ya Afrika Mashariki 1977.

Hii jumuiya ndiyo iliyokuwa inamiliki kwa pamoja  Shirika la Ndege la Afrika Mashariki yaani East African Airways EAA.

EAA ilikuwa na makao yake makuu Jiji la Nairobi Kenya na hivyo miundombinu yote muhimu ya uendeshaji ilikuwa huko na hata wafanyakazi wengine kutoka ndani ya nchi wanachama walikuwa wakiishi Nairobi.

Baada ya kuvunjika ghafla kwa EAC, Kenya ilizuia ndege  zote isipokuwa nadhani ndege mbili au moja ambayo ilikuwa Kwenye Anga ya Tanzania wakati inatangazwa jumuiya imevunjika.

Ndege hiyo ilikuwa Fokker Friendship F-27.
Kimsingi Tanzania tulijikuta tunaamka asubuhi hatuna huduma ya usafiri wa Anga.
 haraka Rais Nyerere alimteua Jaji wa Mahakama Kuu Mh Yahya Rubama kuongoza kikosi kazi cha kuanzisha ATC na kuweza kupata ndege kadhaa ndani ya muda mfupi.

Kazi ilikuwa ngumu sana. Ndege hizo zilipatikana kwa njia ya mkopo na serikali wakati ikiendelea kuimarisha mtaji wa ATC mwaka1978 tukaingia kwenye vita na Uganda hali ambayo iliteteresha uchumi wa nchi yetu lakini ndege za ATC zilitoa mchango mkubwa wakati wa vita.

Baada ya vita hali ya uchumi iliendelea kuwa ngumu kwa waliokuwepo watakumbuka ugali wa Yanga, uhaba wa bidhaa nk. Hivyo basi ATC nayo ilipitia wakati mgumu sana kimtaji na pia kiuendeshaji.

 Lakini bado tuliweza kuhhimili na kuendeleza sekta ya anga na ATC ikiwa Ni mhimili mkubwa kwa kutoa huduma na mafunzo katika nyanja mbalimbali ikiwemo marubani, mafundi, nk

Miaka kadhaa baadae, wakati nchi yetu ikiendelea na jitihada za kufufua uchumi, Bank ya Dunia na Shirika la Fedha duniani vilisimamia urekebishaji wa sera zetu na kutaka serikali ijiondoe kwenye kufanya biashara na badala yake ijikite kwenye kukusanya kodi, biashara iachiwe sekta binafsi. Sera hii ya benki ya dunia na shirika la fedha duniani walikuja na mpango uitwao Structural Adjustment Program mpango huu ndio ulioshinikizwa sana na mataifa ya magharibi kuwa lazima utekelezwe

Hapa ndio mwanzo wa kufa kila kilicho cha serikali.

Hapo ndiyo mwanzo wa sera ya taifa ya ubinafsishaji iliponza na kutakiwa kuyabinafsisha mashirika ya umma.
Mashirika kadhaa yaliwekwa sokoni ikiwemo ATC.

Mashirika kadhaa yaliwekwa sokoni ikiwemo ATC chini ya usimamizi wa Tume ya Rais ya Urekebishaji wa Mashirika ya Umma yaani PSRC na hapo shughuli zote za Standing Committee  on Parastatal Organizations (SCOPO) ilikoma kufanya kazi.

Pamoja na mambo mengine, shirika litakalo kuwa specified kwa ubinafsishwaji likiwekewa masharti maalum kwa mfano

 ATC katika kipindi chote likisubiria ubia na halikutakiwa kufanya  single investment inayozidi USD 1Million. Kwa sekta ya anga uwekezaji wa USD 1m Ni mdogo sana na ATC ilikuwa kwenye kipindi hicho cha kusubiri ubia kwa muda mrefu sana na haikuweza kupata ubia hadi inavunjwa mwaka 2002.

Matokeo yake nini, ni kwamba mtaji wa ATC uliendelea kudumaa na kusababisha iendelee kupata hasara zaidi na zaidi.

Mwaka 2002 serikali ilisitisha ATC ambayo ilianzishwa 1977 kwa sheria ya Bunge ambayo haikuwa inaruhusu umiliki wa pamoja na sekta binafsi na hivyo kuanzisha Kampuni ya Ndege ya Tanzania yaani Air Tanzania Company Limited kwa kutumia sheria ya makampuni yaani Company Ordinance Chapter 212.

 ATCL baadae iliuza 49% ya hisa zake kwa South African Airways December 2002. Baada ya hapo SAA walipewa jukumu la kuendesha menejimenti ya ATCL lakini kutokana na mgongano wa kimaslahi ATCL ilidhoofishwa na kufikia maamuzi ya serikali ya kuzinunua tena hisa 49% na kuiweka katika umiliki wa 100%.

Hivyo basi unazoziona sasa Ni juhudi za kulifufua shirika hilo Nadhani hatutakiwi kuzibeza bali kuunga mkono.

Muda ni mwalimu wetu mzuri, hutufundisha mengi mazuri na kututaka kuendana nayo.

Nyakati zimebadilika sana hasa kwenye biashara ya usafiri wa anga. 1977 ATC inaanzishwa hakukuwepo na Emirates wala Etihad au Qatar Airways. Haya mashirika matatu ni makubwa sana kiasi cha kuweza kuyaweka kwenye wakati mgumu kibiashara mashirika makubwa na kongwe kama British Airways, Sabena, Alitalia, Lufthansa, KLM, Air France, Swiss Air nk.

 Baadhi ya mashirika ya ndege yamefutika na mengine yamejipunguza. Kwa mfano mashirika kongwe yanayokuwa Dar sasa hivi KLM na Swiss nadhani mengine yameshindwa ushindani.
Pili, Nairobi ni saa moja tu kutoka Dar na ni kitovu kikuu cha usafiri wa anga hapa Africa Mashariki hivyo basi operators wengi wa safari ndefu wanaamua kuishia Nairobi zaidi maana yake Nairobi ina wasaa mkubwa kulinganisha na Dar.

Hivyo basi unapotaka kuanza safari za mbali lazima uingie kwenye hasara.

Tanzania yaani nchi yetu ina safari za ndani nyingi sana kuliko nchi nyingine  kusini mwa Africa ukiitoa South Africa. Hivyo basi hizi safari za ndani  Ni fursa, ni soko ambalo hatuna ushindani na mashirika ya nje, tuna uwezo wa kulijenga na kuliendeleza tunavyotaka.

Serikali kwa kuliona hilo imeendelea na uimarishaji wa viwanja vya ndege nchi nzima, kutoka Pemba hadi Sumbawanga, kutoka Bukoba hadi Mtwara. Ili kulikamata soko hili la ndani Ni lazima uwe na zana zitakazoweza kuhudumu viwanja vingi zaidi, Q400 Ni jawabu.

Wakati wa ATC zilikuwepo DHC Twin Otter kwa ajili ya viwanja kama Sumbawanga Nachingwea, Kilwa, Mafia, Iringa, Pemba, Bukoba, nk
F27 ilikuwa ikihudumu baadhi ya hivyo viwanja pamoja na viwanja vingine kama Zanzibar, Tanga, Mtwara, Lindi, Dodoma, Tabora, Kigoma, Mwanza, Shinyanga, Musoma, Kia, Kigali, Bujumbura, Mombasa, nk

B737 ilihudumu Zaidi Kia Mwanza, Zanzibar, Mtwara, Johannesburg, Lusaka, Lilongwe, Nairobi , Entebbe, Iilongwe, Dubai, Muscat, Aden,

Tuiunge mkono serikali kwa kuhakikisha shirika hili linafanya kazi kwa ufanisi.

Mwandishi

Isaac Kitogo

Imekusanywa na kufanyiwa majumuisho na

 Amarison Tanga Tanzania

Monday 5 September 2016

IJUE AMARISON CONSULTANCY


Amarison ni wataalam wa ushauri wa kitaalamu juu ya masuala mbalimbali ya kibiashara.Lengo kuu ni kutoa  ushauri wa kitaalamu utakaomuwezesha mteja wetu kuweza kuiendea biashara yake katika mafanikio ya hali ya juu kwa weledi na ufanisi unaoleta tija.

Ushauri wetu umejikita zaidi katika fani zote za kitaalamu ambazo kwa asilimia kubwa ni hitajio kubwa la kwenye jamii ya mwanadamu.Ushauri unaotolewa huwa ni siri baina yetu na mteja.Kuhifadhi siri ya tunaowahudumia ndio jukumu letu kuu na la msingi.

Katika harakati za maisha ya kila siku binaadamu huwa na shughuli mbalimbali za maendeleo.Shughuli hizo huchangia kwa kiwango kikubwa katika kujenga na kuendeleza taifa.Wakati mwingine mwanaadamu hukwama na kuhitaji ushauri ili kuweza kufanikisha azma yake hiyo.Amarison tupo kwa ajili hiyo.

Kutokana na utafiti tulioufanya tumebaini kuwa kuna aina kuu nne za watu katika jamii katika harakati za kujiletea maendelo.Makundi hayo tunaweza kuyagawa katika muktadha huu:-

1. Watu wenye mawazo ya biashara,

Katika jamii tunayoishi kuna watu wengi sana wana mawazo          mengi ya kibiashara, wana mipango mingi ya kibiashara, ila wamekwama na hawajui wapi na ni kwa vipi waanzie.Hili ni kundi la kwanza ambalo AMARISON tupo kwa ajili yao.Jukumu letu ni kuwaonesha njia ni namna gani wanaweza kuyatoa mawazo yao kutoka katika nadharia na kuyapeleka katika utendaji.

2.Watu waliokata tamaa na maisha

Katika maisha ya mwanadamu kuna mambo mengi sana ambayo humtokea katika maisha ya kila siku na aghalabu wakati mwingine humfikisha mahali mwanadamu hukata tamaa na hata kuona kuna haja ya kuondoka duniani na kuhisi haoni sababu ya kuishi tena kwa namna alivyoharibikiwa au alivyokata tamaa.AMARISON tupo kwa ajili ya watu wa namna hii kwa kuwarejeshea matumaini mapya na kuamsha ari za ndoto zao walizohisi zimekufa na kupiga hatua zaidi.

3. Wafanyabiashara wanaoshindwa kufikia mafanikio 

Katika jamii ya mwanadamu kuna watu hujishughulisha na shughuli za biashara na hushindwa kupiga hatua katika biashara yake kutoka sehemu ya chini kwenda sehemu ya juu zaidi kwa kuongeza au kutanua wigo wa kibiashara na hata wakati mwingine shughuli zake huyumbayumba na hata hufikia mahali hutamani kuachana na biashara zake kwa vile zinavyomuumiza kichwa.AMARISON ipokwa ajili ya kundi hili kuhakikisha wanakuwa na ustawi bora wa kibiashara na kufanya biashara kwa ufanisi wa hali ya juu kuliko hapo awali.

4.Watu wenye rasilimali zote ila waoga wa kuthubutu

Katika jamii ya mwanadamu kuna kundi la watu ambalo hilo lina rasilimali fedha pamoja na nyenzo nyingine za kuendea shughuli za kibiashara lakini wamekuwa waoga sana kiasi cha kuhofia kuwekeza chochote wakifikiria kupata hasara na hela zao kupotoea.Watu hawa wapo ila wamekwama kwa kukosa ujasiri wa kuthubutu.AMARISON ipo kwa ajili ya watu aina hii kwa ajili ya kuwajengea uwezo na kuingia katika shughuli za kibiashara kwa mafanikio na ufanisi.

Amarison ndio suluhisho lako hujachelewa anza sasa.
wasiliana nasi kupitia mawasiliano yetu hapo juu.
Ahsante.