Monday 10 October 2016

KUTOKUWA NA AJIRA NI TATIZO LA" MTAZAMO POFU"


Mtazamo pofu ni aina ya mtazamo ambao mtu anakuwa hana uwezo wa kuona jambo zaidi ya upeo wake wa ziada bali huweza kuliona jambo katika mtazamo mmoja tu.

Jamii na kila mwanajamii analalamika kuwa hana ajira.Kilio hiki ni kikubwa sana kwa vijana wasomi kwasababu wao wanaamini zaidi juu ya ajira ya kuajiriwa na si kujiajiri.

Iwapo utawahoji na kujadiliana nao juu ya ajira ya kujiajiri basi jambo moja kuu litakalokuwa kikwazo kwa vijana wasomi watakwambia hawana mtaji.Wakimaanisha mamilioni ya hela ya kuweza kufanya biashara.

Mtazamo pofu huanzia pale mtu anapoitazama ajira kuwa ni lazima uwe umeajiriwa sehemu fulani uko kwenye kiti cha kuzunguka una nesanesa na kupulizwa na kiyoyozi ila hana imani juu ya ajira ya kujiajiri.

Mtazamo pofu pia hujitokeza pale unapotazama mtaji kuwa ni hela ya kuanzia biashara huu nao ni mtazamo pofu maana umeshindwa kuweza kuona yaliyokuwepo zaidi ya hapo.

Angalia maisha ya vijana waliohitimu vyuo vikuu wanavyohangaika kutafuta kazi huku wakiwa tayari kichwani wana maarifa yenye nadharia nyingi na mipango mingi ya mafanikio ila wameshindwa kuamua kutekeleza kivitendo maarifa hayo ili yawapatie kipato.

Tazama vijana walioishia kidato cha 4 au cha 6 wako mtaani wakifanya biashara zao na wanaendesha maisha yao kwa ufanisi tu,  msomi ana hahaha mtaani kutafuta kazi huu ndio upofu.

Niliamua kuchukua muda katika maisha yangu kuanza kulifanyia utafiti haswa kwa hawa vijana ambao wao hawakufikia elimu ya juu ila  wengi wao ndio wafanyabiashara na ni wajasiriamali huku wasomi wakibaikia katika hatua ya kuajiriwa na hao na kulia njaa kila baada ya siku.

Kitu nilichokibaini ni kuwa, vijana hawa ambao hawakufika elimu ya juu wao wana uthubutu ujasiri subra na uvumilivu saana katika kuyaendea maisha yao na wana nidhamu kubwa ya matumizi ya pesa kwasababu wanajua ugumu wake na kupatikana kwake kwa namna wanavyoitafuta katika biashara zao za kila siku.

Kitu kingine ambacho nimekigundua kutoka kwa vijana ambao ni wafanyabiashara na hawakufikia elimu ya juu kuwa wao wanaishi maisha yao halisi si maisha ya kutaka kuonekana kuwa ni watu wa hali flani ya juu kimaisha ambapo matumizi yao yamekuwa ni ya wastani na muda mwingi hufikiria zaidi kuwekeza katika fursa nyingine za kibiashara.

Jambo la mwisho nililolibaini ni kuwa wao kila fursa wanaiona ni njia ya kuitumia kujipatia kipato cha halali.Nilipojaribu kuwahoji na kuuliza asilimia kubwa kati yao wakati nikiwauliza mwanzo wa biashara zao walinijibu uaminifu ndio mtaji wake alioanza nao ambapo mpaka leo analetewa mizigo anauza na kulipa kama kawaida.

Wakati msomi akihangaika na business plan na maandiko mradi kutafuta wadhamini na wahisani huku akiamini juu ya mtaji pesa tayari kuna ambao wao wameanza na mtaji uaminifu.

Yupo aliyenisimulia maisha yake kuwa yeye aliamua kuchukua bidhaa kwa mtu na kuanza kusambaza katika maduka na katika kila bidhaa aliyokuwa akisambaza yeye alikuwa akiongeza shilingi 1000 au 500 ambapo leo hii ana miliki duka kubwa sana la simu na vipodozi katikati ya jiji la Dar es salaam.

Kila ukimuuuliza jibu atakwambia kaka mimi sijasoma nimeishia kidato cha 4 ila uaminifu ndio umenifanya nimefika hapa.Hakika ukisikiliza historia zao watu hawa unaiona tofauti kubwa sana kati ya kijana msomi na kijana aliyeishia kidato cha nne katika uthubutu wa kujaribu na kujiajiri.

Duniani kote inaonesha dhahiri kuwa sekta ya ajira ya kuajiriwa iwe ni serikalini au sekta binafsi ni 25% tu kila mwaka wanaoajiriwa kutoka kwa waliohitimu katika kila nchi katika sekta zote.Je 75% inakwenda wapi? Hapa ndipo unapoiona sekta ya kilimo na ufugaji ikisubiri 75% sekta ya uvuvi ikisubiri 75% sekta ya ujasiriamali  na uchuuzi ikisubiri asilimia iliyobaikia.

Katika mazingira haya ndipo unapoona mtazamo pofu wa kuiona ajira ya kuajiriwa na kutokuiona ajira ya kujiajiri hatimaye kila msomi huililia serikali kutoa ajira.

JUKUMU LA SERIKALI dunia nzima ni kujenga miundombinu bora na imara ya raia wake kuweza kupata maarifa yaani elimu itakayowawezesha wao kuzikabili changamoto zilizopo katika mazingira yao na sio kuajiriwa.Ikiwa umehitimu shahada ya kwanza na mpaka leo unahangaika kutafuta ajira na huzioni fursa za wewe kujiajiri basi jua pamoja na elimu yako na wewe una mtazamo pofu.

Duniani hakuna serikali inayoajiri 100% katika 25% hugawana na sekta binafsi sasa wewe unayesubiria kuajiriwa utasubiri sana maana wapo wengi kama wewe wanaendelea kulia na kusota mtaani wamebakia kujisifu kuwa wamesoma sana.Wamebaikia na vyeti wakiviangalia kama picha na kuvisoma kama magazeti.

Acha kujidanganya na hivyo vyeti sekta ya kujiajiri haingalii mivyeti yako inaangalia upeo na akili yako ya kuweza kuyaona maisha nje ya mtazamo wa darasani ulipokuwa ukisoma.

Ukitaka kujiajiri sahau kwa mda habari za degree yako huku mtaani kwenye kujiajiri hiyo haina nafasi kwa mwanzo utakuja kuitumia mbeleni.Ile elimu uliyoipata ambayo ipo kichwani kwako ndio sasa inatakiwa ikuoneshe namna gani unaweza kuziona fursa na kuziendea.

kumbuka : HUSOMI ILI UAJIRIWE UNASOMA KUFUTA UJINGA NA UPUMBAVU ili uweze kupata maarifa yatakayokuwezesha kukupa mbinu bora ya kuzikabili changamoto za maisha yako.

KAMA ULISOMA KWA MTAZAMO HUU WA KUAJIRIWA UJUE UNA MTAZAMO POFU

Makala hii ni kwa ajili ya wewe ambaye mpaka leo unasubiri kuajriwa.

NINI CHA KUFANYA kuondokana na mtazamo huu pofu endelea kufuatilia

www.amarisontanga.blogspot.com 

kwa elimu zaidi.

No comments:

Post a Comment